Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Dkt. Alaa Abdulhasan Al-Zughaybi, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Baghdad, amesisitiza kuwa tamasha la 11 la kitamaduni la «Al-Siddiqah Al-Tahirah (s.a.)» ni fursa ya kujifunza na kupata msukumo kutoka katika tunu za kibinadamu na kimaadili, pamoja na kuimarisha maana ya kushikamana na utambulisho wa kitaifa.
Kauli hizo zilitolewa wakati wa shughuli za tamasha hilo lililoandaliwa na Tawi la Mahusiano ya Vyuo Vikuu na Shule, lililo chini ya Idara ya Mahusiano ya Umma ya Ataba Takatifu ya Abbasiyya, kwa ajili ya kuadhimisha kumbukumbu ya kuuawa kkshahidi Bibi Fatimah Zahraa (s.a.), kukumbusha mwenendo wa maisha yake pamoja na tunu za imani, elimu, kujisitiri na kusimama imara katika misingi aliyokuwa akiisimamia.
Kuanzia usafi wa moyo na subira hadi sauti ya haki: Kudhirika kwa mwenendo wa Bibi Zahraa katika harakati za Imam Hussein (as)
Al-Zughaybi alisema kuwa; Chuo Kikuu cha Baghdad kina furaha kubwa kuwa mwenyeji wa mkusanyiko huu unaohuisha kumbukumbu ya shakhsia ya Bibi Fatimah Zahraa (s.a.) na nafasi yake katika historia ya Uislamu.
Alieleza kuwa Bibi Fatimah Zahraa (s.a.) alikuwa mfano bora wa usafi wa moyo, imani na subira; alikuwa sauti ya haki katika nyakati ngumu, na alikuwa shule ya malezi, uelewa na uwajibikaji, ambayo athari zake zimeendelea kuenea katika vizazi mbalimbali. Tunu hizo zilidhihirika katika mwenendo wa maisha ya watoto wake na misimamo yao isiyosahaulika, hususan katika harakati za Imam Hussein (as), ambazo zilikuja kuwa alama ya kujitolea mhanga na kusimama imara katika misingi.
Aliongeza kuwa; kuhuisha kumbukumbu hii hakuishii tu katika kurejelea tukio moja la kihistoria, bali ni fursa ya kupata msukumo kutoka katika tunu za kibinadamu na kimaadili ambazo Bibi Fatimah Zahraa (s.a.) alizidhihirisha. Vilevile, ni fursa ya kuimarisha maana za ikhlasi, uelewa na kushikamana na utambulisho pamoja na tunu za kiroho na kitaifa katika nafsi za vizazi mbalimbali.
Wajibu wa chuo kikuu si kutoa elimu pekee, bali pia kujenga utu na kuimarisha uelewa wa kitamaduni na kimaadili
Al-Zughaybi alibainisha kuwa; jukumu la chuo kikuu haliishii katika kufundisha na kutoa elimu pekee, bali linapanuka hadi katika kujenga utu wa mwanadamu, kuimarisha uelewa wake wa kitamaduni na kimaadili, pamoja na kusisitiza tunu zinazohifadhi utambulisho na uhalisia wa jamii.
Mkuu huyo wa Chuo Kikuu cha Baghdad alitoa shukrani kwa hatua iliyochukuliwa na Ataba Takatifu ya Abbasiyya ya kuwaenzi wanafunzi wa kike wanaoshikamana na uvaaji wa vazi la Kiislamu, kama ishara ya kuthamini msimamo wao wa kushikamana na Hijabu na tunu halisi za Kiislamu, jambo linalodhihirisha fahari yao juu ya utambulisho wa kitamaduni na kidini wa jamii.
Mwisho wa hotuba yake, alitoa shukrani na pongezi kwa Ataba Takatifu ya Abbasiyya kwa juhudi zake za kuandaa tamasha hili la kila mwaka. Alisisitiza kuwa Chuo Kikuu cha Baghdad kinatilia maanani kuandaa na kuwa mwenyeji wa shughuli za kitamaduni na kidini zinazochangia kuimarisha uelewa na kuzipandikiza tunu za kibinadamu na kimaadili katika jamii.
Maoni yako